Saudi Arabia imesema Falme za Ghuba zimelikubali ombi la rais wa Yemen Abedrabbo Mansour Hadi kuandaa mazungumzo mjini Riyadh yanayonuiwa kusaidia kuikwamua nchi hiyo kutokana na mzozo wa kisiasa. Rais Hadi, ambaye anaendesha shughuli zake katika mji wa kusini wa Aden tangu alipoukimbia mji mkuu Sanaa mwezi uliopita, aliliwasilisha ombi hilo kwa mfalme Salman wa Saudi Arabia baada ya kushindwa kuafikiana na wapinzani wa kishia na washirika wao kuhusu mahala pa kufanya mkutano huo nchini Yemen.
Ofisi ya katibu mkuu wa baraza la Ushirikiano wa Mataifa ya Ghuba imesema itafanya maandalizi yanayohitajika kufanikisha mazungumzo hayo, ambayo tarehe yake haijatangazwa. Wakati huo huo, Jamhuri ya kiislamu ya Iran imeonya leo kwamba Yemen iko katika hatari ya kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe huku ikimlaumu rais Hadi kwa kusababisha mzozo ulipo nchini humo.